title : MIAKA SITA BILA KABEYA BADU
kiungo : MIAKA SITA BILA KABEYA BADU
MIAKA SITA BILA KABEYA BADU
Na Moshy Kiyungi
Kabeya badu alikuwa mwimbaji mahiri katika bendi ya La Capitale, aliyewaacha wapenzi na mashabiki wa muziki wa dansi hapa nchini, wakiwa bado wanamhitaji.
Mwaka huu ametimiza miaka sita atngu aiage dunia Machi 06, 2013 akiwa katika hospitali wa Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa maradhi ya figo, akiwa amefikisha umri wa miaka 68.
Mpaka alipofikwa na umauti, alikuwa ni mwanamuziki mwenye vipaji vya kutunga na kuimba katika bendi ya La Capitale ‘Wazee Sugu’ inayoongozwa na mkongwe Kikumbi Mwanza Mpango ‘King iki’.
Msimba wa Kabeya uliwatia simanzi na majonzi makubwa waombolezaji waliofika katika hospitali ya Muhimbili kuuaga mwili wake na katika mazishi yaliyofanyika katika makaburi ya Kinondoni Machi 07, 2013. umati wa watu walibubujikwa machozi mara walipoona mwili wake ukishushwa kaburini.
Kabeya Badu toka alipoanza safari yake katika muziki, kamwe hakuwa mtu mwenye soni, alikuwa tayari kuiacha bendi na kwenda nyingine wakati wowote, ili mradi maslahi yawe mazuri. Alipitia bendi nyingi akiwa huko kwao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na hapa Tanzania, ambapo alipigia katika bendi si chini ya tano tofauti.
Si vyema kumsifia mtu baada ya kufa, lakini kwa Kabeya ninalazimika kufanya hivyo kwa kuwa mwishoni mwa mwaka jana 2012, nilipata fursa ya kufanya mahojiano naye ili kujua Wasifu wake.
Nilizungumza na Kabeya Badu kwa takribani saa mbili mfululizo, akinisimulia historia ya maisha yake kwa ujumla. Aliaza kwa kutaja majina yake akisema anaitwa Kabeya Chibangu Badu, alizaliwa Januari 22, 1945 katika mji wa Likasi, huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Elimu ya msingi alipata katika shule ya Ecole Officialle Laique de Kolwezi, akamaliza mwaka 1959.
Kabeya alisema muziki alianza kuupenda tangu akiwa bado mdogo na alipopata umri wa kwenda kanisani, alijiunga katika kwaya akiimba nyimbo injili. Akiwa kanisani humo, alijifunza jinsi ya kutengeneza ‘Melody’ baadaye mwaka 1963, akajiamini kwamba anaweza kufanya muziki. Alikwenda kujiunga na bendi ya muziki wa dansi ya Ricco Jazz, iliyokuwa katika wilaya ya Kolwezi. Akiwa huko Kabeya alijiunga na chuo cha ufundi ambako alichukua masomo ya useremala na uashi.
“tangu nikiwa mdogo, nilipenda sana nyimbo na uimbaji wa Tabu Ley Rochereau na Kabasele Yampanya ‘Pepe Kale’ nikatamani siku moja nifikie hadhi yao…” anasema Kabeya. Familia yake ilijitahidi kumpa moyo ili aweze kufanya vizuri katika muziki, hivyo ilimshauri kabeya kujifunza lugha ya Kifaransa ambayo inazungumzwa nchini mwao.
Kabeya alikubaliana na ushauri huo, akaingia katika chuo kilichokuwa kikimilikiwa na dhehebu la dini ya Protestant huko Kananga, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kiu cha Kabeya kilipozwa pale alipopokea cheti baada ya kufuzu somo hilo la Kifaransa. Harakati za kutafuta maisha zilimfikisha kufanya kazi katika gazeti moja la Reality Congolese la mjini Kananga, kwenye kitengo cha usambazaji mwaka 1967.
“Baada ya miaka miwili kupita, mmiliki wa gazeti hilo alikamatwa baada ya gazeti hilo kuandika habari zilizo muudhi rais wa wakati huo Mobutu Seseseko, hatima yake gazeti likafungiwa, tukakosa kazi….” anaeleza Kabeya Badu.
‘kuvunjika kwa koleo si mwisho wa ujenzi’ msemo huu aliufanyia kazi Kabeya ambaye mwaka huo huo alianza safari yake ya muziki kikamilifu. Akajiunga katika bendi ya Lupe Jazz, baadae akaenda katika bendi nyingine ya Amide Success. Kabeya hakuishia hapo kwani aliondoka tena na kwenda kujiunga na bendi ya Santa Fee, baadae akajiunga katika bendi ya Lupina Nationale, ambako alikutana na Kasongo Mpinda ‘Clayton’ huko Kananga.
Utulivu katika bendi kwake haukuwepo kabisa, kwani aliondoka tena na kwenda kujiunga katika bendi ya Lupe Revolution, iliyokuwa ya vijana kama yeye. Jina na sifa za uimbaji wake zikazagaa kila pembe. Ndipo alipochukuliwa na Omer Baba Gaston Ilunga wa Ilunga, akajiunga katika bendi yake ya Baba Nationale Septemba 1968. Mwaka 1970, Kabeya alishawishika kwenda kutafuta ajira katika mji wa Kinshasa. Huko alibahatika kupata ajira katika bendi ambayo baadae akagundua kwamba ilimpa ahadi za uongo za maslahi, naye akaachana nayo.
Kati ya mwaka 1971 na 1972 Kabeya Badu alipiga muziki katika bendi ya Festival du Zaire katika jiji la Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kabeya alirudi Likasi mwaka huohuo wa 1972 na kujiunga na bendi ya Fouvette ambayo baadae ilibadilishwa mnajina ikaitwa Safari Nkoi. Alikuwa ni mwanamuziki Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’ aliyemuita kwenda kujiunga katika bendi hiyo.
Hapo alikutana na wanamuziki wengine magwiji Ndala Kasheba na Baziano Bweti. Kabeya Badu nasema kwamba alisoma darasa moja na Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’, katika shule ya msingi ya shule ya Ecole Officialle Laique de Kolwezi, ambako walimaliza masomo yao mwaka 1959.
“Tangu tukiwa vijana tulikuwa tukielewana sana na Kiki. Ndiyo sababu nimekuwa naye sambamba tukienda sehemu mbalimbali hadi leo ninaye…” alisema Kabeya. Walipokuwa Kolwezi wakipiga muziki katika bendi ya Safari Nkoi, walikuwa wamepanga nyumba moja, walichangia bajeti ya chakula kwa pamoja kila mwisho wa mwezi.
Mwaka 1973 uongozi wa Safari Nkoi ulianza kuwafanyia ‘mtimanyongo’ wanamuziki wake akiwemo ‘King Kiki’ lakini Kiki, aligundua mapema hali hiyo. Akamshawishi Kabeya mwaka huohuo wa 1973, kuondoka na kwenda kuanzisha bendi yao.
‘mwenye bahati habahatishi’ msemo huo ulijionesha dhahiri kwani kabla hawajaazisha bendi yao, akajitokeza tajiri mmoja aliyejulikana kwa jina la Paradizo, akimtaka Kiki kwenda Lubumbashi kuanzisha bendi yake. “Kiki hakuniacha mwaka 1974 tukaenda Lubumbashi kuunda bendi ya tajiri huyo ya Buka Buka Mabele. “Ukiritimba wa tajiri ulisababisha bendi hiyo kufa baada ya miezi sita…” alielezea mwanamuziki huyo.
Kabeya akaongeza akisema baada ya kufa kwa bendi ya Buka Buka Mabele, Kiki mwaka 1974 mwishoni aliamua kwenda mji mkuu wa DRC wa Kinshasa. Lakini kabla hajaondoka, aliwashawishi yeye na wanamuziki wenzake warejee Safari Nkoi. Walikubali ushauri hou nao wakarejea na wakapokewa na uongozi wa Safari Nkoi kwa mara nyingine tena.
Kwa kipindi hicho akiwa Safari Nkoi, Kabeya akawa na mawasiliano ya karibu na Kiki, akimshawishi aendelee kubakia Safari Nkoi kwa hali ya utulivu katika bendi ilikuwa ni imeimarika. King Kiki alirejea Lubumbashi mwaka 1976, akitokea Kinshasa pasipo kumafamamisha mtu yeyote. Kabeya anasema “ tulikuwa tunapiga muziki katika ukumbi mmoja wa Rele Night Club mjini Lubumbashi, ghafla Kiki akapanda jukwaani na kushika ‘Mic’ akaanza kuimba. sote tukabutwaika tukaona kama vile ‘shetani’ aliyetua kimiujiza jukwaani”
Mwaka 1977 Kikumbi Mwanza Mpango alifuatwa na Chibangu Katayi ‘mzee Paul’ aliyetokea Maquis du Zaire iliyokuwa hapa nchini. Kiki alimuuliza mzee Paul iwapo wanamuziki waliopo Maquis du Zaire wanakidhi viwango? mzee Paul alijibu kwa wasiwasi na kupendekeza bora kuchukua wanamuziki huko drc. Kiki alipendekeza wanamuziki wa kuondoka nae kuj Tanzania akiwemo Kanku Kelly, Mutombo Sozy, Ilunga Banza ‘mchafu’.
Wakiwa safarini kuja nchini walipitia mji wa Kamina ambako walimpata mnenguaji mwanadada Ngalula Tshiandanda aliyekuwa akinengua katika bendi ya Sakayonsa ya mjini humo. Kabeya badu alikuwa akiwasiliana na King Kiki, akamuahidi kwamba atajitahidi aje Tanzania.
Ahadi ya Kiki kwa Kabeya ikatimia baada ya kufika Maquis du Zaire, ambako alibaini kuwa safu ya uimbaji ikaonekana kupwaya. Aipendekeza kuongezwa kwa wanamuziki zaidi ili kuimarisha bendi hiyo ya Maquis du zaire. Chibangu Katayi ‘ mzee Paul’ kwa mara nyingine tena akatumwa kwenda congo kuwaleta wanamuziki waliopendekezwa na Kiki.
“ tulichukuliwa mimi Kabeya Badu na Kalala Mbwebwe, tukiwa ni watunzi na waimbaji, Monga Kiyombo aliyekuwa na uwezo wa kupiga gita la rhythm na saxophone. Wengine waliochukuliwa ni Ngoi Mubenga kwa upande wa tarumbeta na Khatibu Iteyi Iteyi aliyekuwa mpulizji wa saxophone tukaletwa tanzania mwaka 1978…” alitamka Kabeya.
Kabeya alisema mara alipotua Maquis du Zaire, alitunga na kuimba nyimbo nyingi, baadhi yake ni “Ndoa ya kwangu na mama Kazi”, ‘Pondamali’, ‘Kibwe Mutombo’ na zingine za Muntanda Muli, Lwembe na maneno, ambazo hazikuwahi kurekodiwa.
Kabeya Kadu alipiga na Maquis du Zaire kwa miaka miwili, mwaka 1980 alichoropoka na kwenda akijunga na King Kiki katika bendi ya Orchestra Safari Sound (OSS) iliyokuwa ikimilikiwa na mfanyabiashara maarufu Hugo Kisima. Akiwa na OSS, Kabeya alitunga na kuimba nyimbo za Nani atashika Jembe na Pole ndugu.
Alieleza kuwa wimbo wa ‘Yuyu’ ulipigwa na kurekodiwa katika kipindi cha Klabu raha leo show kilichokuwa kikirushwa na Radio Tanzania Dar es Salaam. (RTD) badu alikuwa akihitajika sana katika bendi hizo mbili pinzani wakati huo za maquis na oss. hivyo akawa mithiri ya ‘muigizaji’ kwa kuhamahama. alirejea tena maquis kwa kipindi kifupi kisha mwaka 1986 akatakiwa kurejea kwa mara nyingine tena katika bendi ya orchestra safari sound.
aliporejea oss tayari bendi ilikuwa chini ya uongozi wa ndala kasheba na haichukua muda mrefu akatoka na wimbo uliowapagaisha wapenzi wa oss wa ziada. wimbo huo aliuimba peke yake kwa hisia kali akimlilia ziada, na ukamuongezea sifa kubwa miongoni mwa waimbaji wa muziki wa dansi hapa nchini. zingine zilikuwa za ‘ kuruthumu’, ‘simba wala watu wamevamia mji’ mama mwita, kayanda na nyingine nyingi.
kabeya badu anamwelezea kikumbi mwanza mpango ‘king kiki’ kuwa ndiye anayejua umuhimu wake na hapa anasema… “ kiki ndiye aliyekuwa akijua umuhimu wangu katika muziki toka mwanzo hadi akanipachika jina la ‘ changa cha mkonyoyo’ ikiwa na maana ya siri iliyofichika…” alipewa jina hilo baada ya kufyatua wimbo wa changa cha mkonyoyo’ anaoulezea kuwa ni ujumbe mzito japokuwa wimbo huo haukuwahi kurekodiwa.
aliondoka oss na kwenda kujiunga kwa mara nyingine tena na maquis du zaire mwaka 1988, hapo napo hakadumu akachukuliwa na kwenda kujiunga na bendi ya tancut almasi iliyokuwa ikipiga muziki wake mjini iringa. ‘msahau kwao mtumwa’ kabeya alitamani kurejea kwao congo, ndipo mwaka 1990 akaamua kurudi kwao likasi katika jimbo la katanga.
kama nilivyokujuza mwanzoni kwamba kabeya alikuwa mtafutaji wa maslahi murua, hivyo alirejea tena tanzania mwishoni mwa mwaka 1998. mwaka uliofuatia wa 1999, akapewa kazi ya kuanzisha bendi ya magoma sound ya jijini dar es salaam. mwaka 2001 alijiunga katika bendi ya la capitale inayoongozwa na kikumbi mwanza mapango ‘king kiki’ au ‘bwana mukubwa’ hadi mauti yake yalipomfika jumatano iliyopita ya tarehe 06 machi, 2013.
kabeya alisema kwamba ana matarajio makubwa anayotamani kufikia. “nina mpango wa kununua vyombo vyangu vya muziki, pia natarajia kurekodi nyimbo zagu zote nilizotunga na kuziimba, nziuze mimi mwenyewe…” anasema kabeya akiwa mwingi wa tabasamu usoni. ninasikitika kwa kusema kuwa kumbe kauli hiyo ikifuatiwa na tabasamu hilo, ilikuwa la ndiyo mwisho, tukiagana naye! kabeya badu alinisisitiza kwamba mara tu makala hii ikitoka, nimualifu ili awahi kununua gazeti hili, lakini mpangaji wa yote ni mungu.
kiongozi wa bendi ya la capitale, kikumbi mwanza mpango king kiki’ alimuelezea kuwa pengo la kabeya kamwe halitazibika. “ kabeya pengo lake halitazibika kamwe ametuachia ukiwa usio na kifani. alikuwa ni mtunzi na mwimbaji mzuri si hivyo tu pia alikuwa msikivu, mtu wa kazi tulishauriana kutengeneza ‘melody’na kwa kwa ushirikiano huo tulikuwa tukichokozana na kutoa vibao ‘matata’ sana. tumempoteza kabeya…” kwa masikitiko na majonzi anasema kiki.
kabeya chibangu badu, ameacha mjane na watoto wanane kati yao watano ni wa kike. wapenzi na wadau wa muziki wa dansi hapa nchini, kamwe hatamsahau kabeya badu kwa jinsi alivyokuwa na uwezo wa kulishambulia jukwa kwa kucheza na kupaza suti yake iliyokuwa nyororo wakati akiimba. Mungu ailaze roho yake pahala pema peponi, amina.
Hivyo makala MIAKA SITA BILA KABEYA BADU
yaani makala yote MIAKA SITA BILA KABEYA BADU Wakati huu, pengine unaweza kutoa faida na wewe wote. Sawa, kuona katika post nyingine makala.
Wewe ni sasa kusoma makala MIAKA SITA BILA KABEYA BADU mahali kiungo https://wordmaelezo.blogspot.com/2019/04/miaka-sita-bila-kabeya-badu.html
0 Response to "MIAKA SITA BILA KABEYA BADU"
Post a Comment