title : Tamko la Asasi za Kiraia Kuhusu Hali ya Usalama Nchini
kiungo : Tamko la Asasi za Kiraia Kuhusu Hali ya Usalama Nchini
Tamko la Asasi za Kiraia Kuhusu Hali ya Usalama Nchini
WITO WA ASASI ZA KIRAIA KUHUSU HALI YA USALAMA WA RAIA, HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA WA SHERIA NCHINI
UTANGULIZI
Sisi Asasi za Kiraia tulioweka sahihi katika Waraka huu, kwa umoja wetu tumesikitishwa sana na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, utawala wa sheria na usalama wa raia vinavyoendelea hivi sasa hapa nchini. Asasi za Kiraia (Civil Society Organizations) ni taasisi huru zilizoundwa kwa mujibu wa sheria mbalimbali nchini. Taasisi hizi zinatekeleza majukumu mbali mbali hapa nchini katika kuhakikisha ustawi wa taifa letu.
Hivyo tunawaomba viongozi na watanzania kwa ujumla kutambua juhudi zinazofanywa na asasi za kiraia katika kutetea maslahi ya umma, kuleta maendeleo na mabadiliko mengine katika jamii. Katika nchi mbali mbali zilizoendelea, mchango wa asasi za kiraia umesaidia kuleta mabadiliko makubwa ya kimfumo na kimaendeleo na hivyo nchi/mataifa husika kuona umuhimu wa kuheshimu AZAKI na kuweka ushirikiano mzuri wa serikali na asasi za kiraia.
Pamoja na changamoto changamoto mbalimbali , AZAKI pia zimetambua na kumpongeza Rais wa Jamhuri wa Tanzania kwa kuonyesha juhudi katika kupamnbana na matumizi mabaya ya rasilimai za umma, kuleta nidhamu katika taasisi za umma na usimamizi mzuri wa mali asili za Watanzania.
AZAKI zitambua kabisa umuhimu wa maendeleo ya kitaifa katika kulinda na kuheshimu haki za binadamu kwa kuwa vitu vyote hivi huenda pamoja na hutegemeana. Kwa maana hiyo tuko bega kwa bega na Rais wetu katika kuhakikisha Tanzania inapata maendeleo makubwa, kwa kuwa maendeleo hayo ndiyo msingi wa haki za binadamu na maisha bora kwa Mtanzania.
TATHMINI YA HALI YA HAKI ZA BINADAMU, UTAWALA WA SHERIA NA USALAMA
Katika utendaji kazi wa asasi za kiraia, huwa zinapata muda wa kukaa na kufanya tathmini ya hali ya mambo mbali mbali ya kitaifa na kuangalia ni namna gani wao kama wadau na washiriki wa kuleta maendeleo na kuhakikisha mustakabali bora wa taifa unalindwa na kutetewa wakati wote.
Mnamo tarehe 19/02/2017 Jukwaa la Wakurugenzi wa AZAKI (Tanzania CSOs Director’s Forum-CDF) Ililikaa kikao ili kufanya tathmini ya masuala mbalimbali yenye maslahi na mustakabali mzima wa taifa hili na kubaini masuala kadhaa ya ukiukwaji wa haki za binadamu, hali ya taharuki juu ya amani ya nchi, uhuru wa kujieleza, uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa AZAKI, maamuzi yasiyozingatia sheria na taratibu, kuminywa kwa demokrasia ya taifa letu pamoja na chaguzi zisizo na usawa na zenye viashiria za umwagaji damuna kuhatarisha amani ya nchi.
Hali hii imetokana na matukio mbali mbali ambayo tumeyashuhudia na kwa kuzingatia historia ya nchi yetu hatukuwahi kuyashuhudia wala kudhani kwamba yangeweza kutokea. Matukio haya yamehusishakuvamiwa (mashambulizi), kuuawawa, kuumizwa, kupotea na kuteswa kwa watetezi wa haki za binadamu, wanahabari, wanasiasa na hata raia wa kawaida. Baadhi ya matukio hayo ni haya yafuatayo;
(i) Mauaji ya Mwanafunzi wa Chuo -Akwlina Baftah
Mnamo tarehe 16/02/2018 taarifa zilisambaa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii juu ya kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Akwilina Baftah ambaye anasadikiwa kuuwawa kikatili akiwa katika daladala na askari polisi waliokuwa wakiwatawanya wafuasi wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambao walikuwa wanakwenda kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kinondoniambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa ajili ya kudai fomu za mawakala wa uchaguzi.
Jeshi la Polisi kupitia kwa Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa, lilithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kukiri kwamba tukio hilo limetokea wakati polisi wakiwa wanafyatua risasi angani kuweza kuwatawanya wafuasi wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Tukio hili limezua taharuki kubwa kwa taifa na jamii ya kimataifa kwani ni moja kati ya matukio mabaya yanayoendelea kutokea katika Taifa letu. Tukio la kuuwawa kwa mwanafunzi huyu limeleta simanzi kubwa sana kwa taifa kwakuwa limetokea kwa mtu asiyekuwa na hatia yoyote ile.
Ni moja ya tukio ambalo limewaleta watanzania pamoja bila kujali dini zao, mirengo yao ya kisiasa, vyeo vyao, makabila yao au hali zao.
Tukio hili limewakumbusha watanzania wengi kwamba kumbe ile amani iliyokuwa ikihubiriwa katika taifa hili inaweza potea ndani ya dakika chache bila kutarajia kama tusipoamka wote kudai Taifa kurudi katika misingi ya demokrasia, usawa, utawala wa sharia na haki za binadamu.
Wana AZAKI tunawashukuru wote wanaoendelea kuifariji familia hiyo hasa Waziri wa Elimu Bi-Joyce Ndalichako alieonyesha ukaribu wa kusimamia msiba huu kama waziri mwenye dhamana ya elimu nchini, lakini pia ushiriki wa Serikali katika kusaidia mazishi ya mwanafunzi huyo.
Wana AZAKI tunawashukuru wote wanaoendelea kuifariji familia hiyo hasa Waziri wa Elimu Bi-Joyce Ndalichako alieonyesha ukaribu wa kusimamia msiba huu kama waziri mwenye dhamana ya elimu nchini, lakini pia ushiriki wa Serikali katika kusaidia mazishi ya mwanafunzi huyo.
Tunaipongeza Serikali kwa kuonyesha kujali na kuwafariji familia ya marehemu kutokana na msaada huo. Sisi kama wana Azaki tunaamini Serikali na wananchi wameguswa sana na msiba huo.
(ii) Vitendo vya kutekwa, kuuwa, kuumizwa na kupotea kwa watu mbalimbali
• Matukio ya kutekwa na kuuwa kwa viongozi mbalimbali hapa nchini yalishika kasi pale viongozi wa CCM, askari zaidi ya 10 na wananchi karibu 40 katika eneo la Kibiti walivyoanza kushambuliwa na kuuwawa bila wahusika kukamatwa. Matukio haya yameendelea hadi kwenye vipindi vya uchaguzi ambapo mnamo tarehe 11/02/2018 Kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ndugu Daniel John alitekwa na kishaaliuwawa kikatili wakati wa Kampeni za Uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni. Matukio haya ni mengi na yamekuwa yakijirudia kote hadi visiwani Zanzibar.
• Tarehe 7/09/2017 Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika na Mbunge wa Singida Mashariki Mhe. Tundu Lissu alivamiwa na kupigwa risasi hadharani na watu wasiojulikana katika eneo la area D Mkoani Dodoma ambapo mpaka sasa watu hao hawajaweza kubainika na.
• Tarehe 21/11/2017 Mwandishi wa habari wa Mwananchi Communications Limited ndugu Azory Gwanda alipotea katika mazingira ya kutatanisha ambapo mpaka sasa hajapatikana licha ya wana AZAKi na waandishi wa habari kupaza sauti zao juu ya kupotea kwake.
• Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ben Saanane alipotea katika mazingira ya kutatanisha na taarifa za wapi alipo mpaka hazijawahi kutolewa na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama wala kuwabaini waliohusika na tukio hilo.
• Matukio ya utekaji na uteswaji wa watu yamekithiri katika nchi yetu ambapo hivi karibuni tumeshuhudia matukio kadhaa ya kutekwa na kuteswa kwa wasanii, wanahabari ambao wanaonekana kutoa maoni mbadala juu ya masuala mbali mbali yanayoendelea katika nchi yetu.
(iii) Matumizi ya Sheria Kandamizi na Ukamataji Usiozingatia sheria
• Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 18 inatoa uhuru wa maoni kwa kila Mtanzania ata hivyo kumekuwa na sheria mbali mbali kama vile Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997, Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015 pamoja na sheria zingine ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikiminya uhuru wa maoni kwa makundi mbali mbali pamoja na watanzania kwa ujumla.
• Tumeshuhudia katika kipindi kifupi cha utekelezwaji wa sheria kandamizi, magazeti mengi yamefungiwa, wanahabari wamevamia, kutekwa na kunyanyaswa, watu kufunguliwa mashtaka ya kughushi, kuvamiwa ofisi za mawakili, vyombo vya habari kupigwa faini kwa kurusha taarifa ambazo pengine zinaonyesha kasoro za uongozi. Hali hii imezua taharuki kubwa kwa tasnia ya habari ambapo sasa wanahabari wanafanya kazi katika mazingira magumu sana na ambayo sio salama hivyo kusababisha kuogopa kutoa taarifa juu ya uvunjifu wa haki za binadamu na mwenendo wa demokrasia nchini.
• Vyombo vya habari vimepigwa marufuku kutoa taarifa za uchaguzi, haza zile zinazonyesha kasoro katika uchaguzi, wengi tumesikitishwa na kitendo cha ITV kutakiwa kuomba radhi kwa taarifa ya kweli waliyorusha wakati wa upigaji kura kwenye uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kinondoni kwa kuonyesha tukio la wizi wa sanduku la kura wakati uchaguzi ukiendelea.
• Utawala wa sheria, Demokrasia na haki za kisiasa vimekuwa havisimamiwi vizuri na vyombo husika. Kwa mfano, Jeshi la Polisi nchini limekuwa likishindwa kutokuwa na upande katika mambo yanayowahusu raia na serikali au vyama vya siasa na hivyo kusababisha madhara na maafa kwa wananchi mbali mbali wa taifa hili.Vyombo hivi vya usalama vinalalamikiwa na wananchi kwa kutokufanya kazi zao kwa weledi, uhuru na usawa na kuonekana kama vinaingiliwa na kufanya kazi kwa maagizo mengi toka nje ya mifumo yao na kuondoa dhana ya kuwa vyombo kwa ajili ya ulinzi wa raia na mali zao.
• Tume ya taifa ya Uchaguzi nchini imejionyesha wazi kuwa siyo chombo huru kinachofaa kusimamia au kuwa msimamizi wa chaguzi za mfumo wa vyama vingi kutokana na muundo wake au wasimamizi wanaoteuliwa kuwa na uhusiano na vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi. Hili limeonekana dhahiri kwamba kuna mambo ambayo tume imeshindwa kuyasimamia wakati wa uchaguzi uliopita na hivyo kusababisha kutokea kwa vurugu na vifo/athari mbali mbali kwa viongozi wa vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla. Kwa mfano, tukio la juzi la kuuwawa kwa mwanafunzi Akwilina Baftah ni matokeo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzina Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni kushindwa kusimamia vizuri zoezi la uchaguzi.
Taarifa zaidi kuhusu uangalizi wa uchaguzi huo zitaletwa baadaye na muungano wa AZAKI zilizoshirikikufanya uangalizi wa uchaguzi baada ya taarifa hizo kukaguliwa kwanza na Tume kwa Mujibu wa taratibu mpya. Hili nalo ni jambo geni kabisa katika taratibu za uangalizi wa uchaguzi ambapo waangalizi walikuwa huru kutoa taarifa zao za uangalizi bila ya kusubiri taarifa hizo kuhakikiwa na TUME.
(iv) Hali ya Watetezi wa Haki za Binadamu na AZAKI
• Watetezi wa Haki za binadamu wameendelea kufanya kazi katika mazingira ambayo sio rafiki na hatarishi huku wengi wao wakifunguliwa kesi, kushambuliwa, kukamatwa na vyombo vya Dola ikiwemo kupewa majina mabaya na hata kuzushiwa kuwa baadhi yao sio raia wa Tanzania.
• Makundi mbali mbali na Asasi za kiraia zimeendelea kufanya kazi katika mazingira ambayo sio rafiki huku uhuru wao wa kufanya kazi na kujieleza ukiwa umeminywa kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria zinazoanzisha na/ama kulinda maslahi ya asasi za kiraia.
• Tumeshuhudia asasi za kiraia zikitishiwa kufungiwa huku zikiwa zinatekeleza majukumu yao kisheria. Nafasi ya asasi za kiraia imedhoofika kutokana na kauli mbali mbali za viongozi wa serikali pamoja na hatua zinazochukuliwa na serikali hivyo kufanya Asasi za kiraia kushindwa kutimiza majukumu yake kwa ufasaha na kwa wakati katika maeneo mablimbali ya nchi.
• Mfano AZAKI nyingi sasa zimekwama kutoa matangazo kwa vyombo vya habari kutokana na kutakiwa kupata kibali kwanza toka TAMISEMI baada ya kuyawasilisha matangazo hayo kwa viongozi kwa ukaguzi. Matangazo kama yale yaliyokuwa yakitolewa na HAKIELIMU kwa utaratibu wa sasa ni lazima kukaguliwa na kupata kibali ndipo chombo cha habari kiweze kuyatoa kwa umma.
• AZAKI zinazokwenda Mikoani kufanya kazi zinakumbana na upinzanimkubwa kutokana na maagizo ya kutaka kupata kibali toka Makao Makuu ya TAMISEMI kabla ya kwenda Mikoani
• Pia AZAKI zinashindwa kutoa taarifa zauangalizi wa uchaguzi kutokana na kutakiwa kupeleka kwanza taarifa hizo kwa Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi kuzikagua ili kuangalia yaliyomo na kuiridhiwa IKIWAPENDEZA. Changamoto hii imeendana na changamoto ya kupata kibali kwa AZAKI kama waangalizi wa uchaguzi. Mfano yapo Mashirika mengine yalikwenda Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuomba kuwa waangalizi lakini walijibiwa kuwa kuna mashirika mengi yameeomba kufanya uangalizi hivyo nafasi zimejaa.
SISI Wana AZAKI tumeona tutumize majukumu yetu kwa kutafuta namna ambayo tunaweza kuijadili kwa pamoja jinsi ya kurekebisha changamoto hizi na kusonga mbele. Tusipofanya hivyo, taifa hili linaweza kuingia katika migogoro ambayo huzaa chuki na hatimaye kupoteza Amani yetu. Kwani kwa sasa kumekuwa na kauli zinazoashiria ubaguzi wa itikadi za kisiasa na kimaendeleo.
WITO WA AZAKI KWA SERIKALI NA TASISI HUSIKA
1. Serikali itazame upya suala la upatikanaji wa Katiba mpya kwani ndiyo suluhisho la matatizo mbali mbali yanayotokea katika jamii kwa sasa, kwani suala la katiba mpya kimekuwa ni kilio kikubwa na hitajio la watanzania wengi ili kutibu hali hii inayojitokeza sasa.Tunashauri Mchakato wa Katiba mpya ufanyike mwaka huu kwa kuwa mawaka 2019 na 2020 Taifa litakuwa bize na mambo ya uchaguzi. Tunamshauri Mhe Rais aitishe kikao cha wadau wote kujadili namna ya kuliweka hili suala kwa maslahi ya Taifa.
2. Tunaomba Tume Huru ya Uchaguzi ipatikane kabla ya chaguzi za 2019 na 2020, itakayoweza kusimamia usawa na haki kwa vyama vyote kuepusha madhara ambayo yanaweza kujitokeza kutokana na Tume kushindwa kusimamia misingi ya haki na usawa katika uchaguzi.Tume ya uchaguzi ifungue ofisi zake wilayani na kuajiri wataalam wake kuwa wasimamizi wa uchaguzi na kuachana na mfumo wa sasa unaonekana kuwa na mgonano wa kimaslahi. AZAKI tupo tayari kushirikiana na Serikali na wadau wengine wa maendeleo katika kulifanikisha hili.
3. Tunapendekeza iundwe Tume huru ya uchunguzi itakayohusisha AZAKI, Taasisi za Dini, Vyombo vya Habari, Baraza la Vyama vya Siasa, Wanahabari, Majaji/Mahakimu, Polisi, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora kufanya uchunguzi huru juu ya vifo na vitendo vya utekwaji na utesaji vilivyojitokeza wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni. Matukio yanayowahusu Polisi kama watuhumiwa ni kosa kubwa kuwaachia wao wenyewe wajichunguze na hili limekuwa sasa chanzo cha matukio kuendelea kutokea na kutochukuliwa hatua.
4. Vyombo vya utoaji haki kama Polisi na Mahakama vifanyiwe maboresho na viachweviwe huru katika kutekeleza majukumu yake ili kuepusha wasiwasi na dhana ambayo imeanza kuonekana dhahiri kwamba vyombo vyetu vya utoaji haki haviko huru. Au kuthibitisha ile zana ambayo imeanza kuzoeleka kuwa kuna Mhimili mmoja umejichimbia kwenda chini kuliko mihimili mingine.
5. Tunalisihi na kulishauri Jeshi la polisi kutimiza wajibu wake kwa kufanya kazi kwa weledi, taaluma na sheria za nchi pamoja na kuacha kuegemea upande mmoja ili kuepusha lawama chuki na uhasama ambao unajengeka kwa wananchi kwa Jeshi hilo.
6. Jeshi la polisi liwe makini katika kutimiza wajibu wake wakati wa kuzuia maandamano, kwani kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na viongozi wa Jeshi la Polisi na matumizi ya silaha za moto huonyesha wazi kwamba Polisi inashindwa kutumia njia zilizoanishwa kisheria kukabiliana na waandamanaji wasio na silaha na wasiofanya vurugu. Pia Jeshi la lifanye kazi kwa ushirikiano na wananchi pamoja na Asasi za kiraia na kwa namna yoyote kuepuka kutumia nguvu kubwa ili kuboresha dhana ya ulinzi shirikishi.
7. Askari wanaotuhumiwa kuhusika kusababisha kifo cha Mwanafunzi Akwilina wafikishwe katika vyombo vya sheria ili hatua stahiki zichukuliwe kwa aliyehusika na tukio hilo. Taifa liwe na mfumo huru au chombo huru (Oversite body) ya kuchunguza na kusimamia mashtaka yanayohusu vyombo vya usalama badala ya kuwaachia wao kufanya uchunguzi na kuendesha mashtaka.
8. Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni ambaye ndiye Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kinondoni ajipime mwenyewe kwa vitendo vyake alivyofanya katika uchaguzi huu kuhusu kuvuruga taratibu za uchaguzi na kuwanyima mawakala wa vyama vingine haki ya kusimamia uchaguzi pamoja na kusababisha uvunjifu wa amani ajipime kama anatsahili kuendelea katika nafasi hizo tena. Viongozi wengine wahusika nao wajitafakari.
9. Tume ya Utawala Bora na haki za binadamu nchini iingilie kati vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu nchini kwa kufanya utafiti huru juu ya yale yanayotokea katika jamii na kupendekeza njia sahihi za kushuhulikia ukiukwaji wa haki za binadamuTanzania.
10. Tunaziomba asasi za kiraia, asasi za kiserikali, wabunge, wanasiasa, mashirika mengine na wadau mbali mbali wa maendeleo kuendelea kupaza sauti na kuungana kwa pamoja kupigania haki, utawala wa sheria, demokrasia na amani ya nchi hii haswa kipindi hiki ambapo kumekuwepo na uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu.
11. Tunashauri kuwepo kwa Mjadala wa kitaifa utakwaowaleta pamoja makundi yote yaliyo kwenye jamii kama viongozi wa dini, taasisi za kitaaluma, vyama vya wafanyakazi, viongozi wa kisiasa, viongozi wa serikali, viongozi wakuu wastaafu na AZAKI ili kujadili amani ya nchi na umoja wetu wa kitaifa ambao uko hatarini kutoweka endapo hatua stahiki hazitachukuliwa.
12. Tunawaomba viongozi wa Serikali waone umuhimu kusikia sauti hizi kwa kutoa nafasi ya majadiliano na kundi hili ili kupokea mapendekezo mengi ambayo AZAKIzinawezatoa mapendekezokwa mustakabali wa Taifa letu.
13. Tunavishauri Vyama vya siasa kuendelea kutumia njia za amani kudai haki zao pale zinapovunjwa wakati AZAKI zinatafuta njia ya amani na ya mazungumzo na taasisi husika na uongozi kwa ujumla.
14. Bunge lirudi katika majukumu yake kama walivyofanya katika matukio ya serikali siku za nyuma kwa kuunda kamati za kibunge kuchunguza hali ya sasa ya utawala wa sheria, haki za binadamu, usalama wa raia na usawa katika jamii.
15. Tunaomba viongozi wa serikali (hasa wale wachache wenye mtizamo hasi kuhusu AZAKI) waone Asasi za Kiraia kama wadau wazuri wa maendeleo na hivyo kuondoa vikwazo vya sasa vinazidi kujitokeza wakati AZAKI zinapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mwisho, sisi AZAKI tunatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa Binti Akwilina na wote waliopoteza wapendwa wao Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi. Amina.
Imetolewa na Jukwaa la Wakurugenzi wa AZAKI Tanzania leo 21/02/2018
Hivyo makala Tamko la Asasi za Kiraia Kuhusu Hali ya Usalama Nchini
yaani makala yote Tamko la Asasi za Kiraia Kuhusu Hali ya Usalama Nchini Wakati huu, pengine unaweza kutoa faida na wewe wote. Sawa, kuona katika post nyingine makala.
Wewe ni sasa kusoma makala Tamko la Asasi za Kiraia Kuhusu Hali ya Usalama Nchini mahali kiungo https://wordmaelezo.blogspot.com/2018/02/tamko-la-asasi-za-kiraia-kuhusu-hali-ya.html
0 Response to "Tamko la Asasi za Kiraia Kuhusu Hali ya Usalama Nchini"
Post a Comment