title : CHADEMA WAMJIBU SPIKA NDUGAI MALIPO MATIBABU YA LISU.
kiungo : CHADEMA WAMJIBU SPIKA NDUGAI MALIPO MATIBABU YA LISU.
CHADEMA WAMJIBU SPIKA NDUGAI MALIPO MATIBABU YA LISU.
*Mkeka wa Spika Ndugai na 'shimo' la barua tatu za vibali matibabu ya Lissu*
Zilipoanza kusambaa habari zikimnukuu Spika wa Bunge, Job Ndugai kuwa amezungumzia suala la matibabu ya Mbunge wa Singida Mashariki na Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu na kwamba Bunge limeshatoa kiasi cha mil. 207 kwa ajili ya matibabu, wengine tulichelea sana kuziamini kwa haraka.
Swali la awali katika kutafuta uthibitisho wa ukweli wa alichokisema lilikuwa ni je, Spika Ndugai ameinasua taasisi ya Bunge kutoka kwenye shimo la barua tatu za vibali kwenye matibabu ya Lissu?
Hivyo basi, kabla ya 'masahihisho' yanayosambazwa kurekebisha nukuu za awali, nilikuwa nimeamua kujiridhisha kupitia Bunge Tv Tanzania, juu ya hasa alichokisema Spika Ndugai ambako nimemsikiliza zaidi ya mara tatu na kumsikia akisema hivi;
"Moja ya madai yake (Lissu) makubwa ni kwamba Bunge hili halijawahi kumjali kifedha...Bunge hili halijawahi kumjali kifedha, toka tarehe saba Septemba, alipopata matatizo yale makubwa ndugu yetu, ambayo tunaendelea kumpa pole.
"Jambo hili amelisemea na kulirudia na kulirudia sana mahali pengi na anaendelea kulisemea. Tutaendelea kutoa ufafanuzi kadri siku zinavyoenda. Lakini itoshe tu kusema kwa Watanzania kwamba Bunge hili kupitia ofisi yangu, kutoka hiyo tarehe 7 Septemba 2017 hadi Desemba, sijajumlisha za Januari, kupitia ofisi yangu, tumeshamlipa... tumeshamlipa Mhe. Tundu Antipas Lissu malipo mbalimbali, ya jumla ya shilingi milioni mia mbili na saba, laki nane na sabini na mbili elfu...malipo mbalimbali...milioni mia mbili na saba, mia nane sabini na mbili elfu. Ukijumlisha na michango yenu kwa ajili ya matibabu ambayo tulilipa Nairobi Hospital mil. 43, ukijumlisha pamoja, tumeshampa ndugu yetu huyu Mil. 250."
"Kwa hiyo kuendelea kusema kila mahali kwamba bunge hili halijawahi kutoa hata senti moja kwa ajili yake katika jambo hili ni jambo la uongo, uongo , uongo kabisa."
"Nalitupa upande wake...nalitupa upande wake, haiwahusu kalipwa yeye sio ninyi... nalitupa upande wake ili akanushe hili sasa ndiyo nitoke na mkeka kamili wa kila kitu," mwisho wa kunukuu.
Ukimsikiliza Spika Ndugai kwa makini, unaweza kubabaishwa na masahihisho yanayoonekana kusambazwa baada ya vyombo vya habari kumnukuu isivyo sahihi (out of context). Ni kweli hakuna mahali ambapo Spika amesema kuwa Bunge limetoa zile mil. 200+ kwa ajili ya matibabu! Neno matibabu amelisema alipozungumzia mil. 43 ambazo zilikuwa ni michango (ya hiari) ya wabunge wao wenyewe binafsi wala si taasisi ya bunge.
Kwanini Spika Ndugai kaamua kuijumlisha hiyo mil. 43 kuwa ni sehemu ya malipo ambayo Bunge (taasisi) limemlipa Lissu kama stahiki zake, pamoja na kuwa sababu hasa anaijua mwenyewe, lakini inafikirisha! Labda alitaka kiwango cha fedha kionekane kikubwa, yaani jumla ya michango ya hisani/hiari ya Wabunge plus stahiki za Lissu, iwe mil. 250!
Jambo ambalo Spika Ndugai anaonekana kulikwepa na hataki kujielekeza huko kwa makusudi ambalo ndilo limekuwa likitawala mjadala wa matibabu ya Lissu ni kuhusu wajibu wa Bunge kumlipia matibabu yake ambayo ni haki yake.
Leo Spika kaamua kutengeneza mjadala mwingine kabisa, ambao unahusu malipo ya mshahara wa Mbunge Lissu na posho zingine za kila mwezi kwa nafasi yake ya ubunge. Stahiki hizo wanalipwa wabunge wote, walioko Bungeni au walioko matibabuni. Sasa hapo nongwa iko wapi! Hizo ni stahiki za Lissu wala SI HISANI ya Spika Ndugai. Hata kutumia maneno 'tumempa' si sahihi kabisa kwa sababu inataka kuonesha kuwa malipp yale yametolewa kama hisani.
Spika alete basi huo mkeka wake tuone utakuwa na jipya gani!
Hata Spika Ndugai mwenyewe alipougua na kulazwa India kwa zaidi ya miezi sita mwaka 2016, alilipwa mshahara na posho zake za kila mwezi. Malipo hayo hayana uhusiano wowote na hela ya gharama za matibabu.
Spika alete huo mkeka wake. Wananchi wanausubiri!
Wakati Spika Ndugai akiuandaa huo mkeka wake uliokamilika, tunaomba akumbuke kujielekeza katika hoja ya msingi kuhusu matibabu ya Mbunge Lissu ambayo ni je bunge limemlipia matibabu Lissu ambayo ni haki yake? Kama tayari, ni kiasi gani? Imelipwa katika akaunti lini na kupitia akaunti ipi? Na je wamelipa baada kwa uthibitisho gani? Kama bado, kwanini amenyimwa haki hiyo?
Tunaweka maswali hayo kwa sababu bado tuna kumbukumbu ya majibu ya Spika Ndugai aliyoyatoa Aprili mwaka 2018, miezi kadhaa tangu Lissu ashambuliwe, akiwa ameshatolewa Nairobi, akiendelea na matibabu awamu ya tatu nchini Ubelgiji, ambapo alipoulizwa kwanini Bunge halijatimiza wajibu wake wa kumlipia matibabu mbunge wake, alisema kuwa;
1. Hawajapata barua ya kibali ya madaktari wa Muhimbili.
2. Hawajapata barua ya kibali cha Katibu Mkuu Wizara ya Afya.
3. Hawajapata barua yakibali cha Rais kuidhinisha malipo hayo.
Alichomaanisha Spika Ndugai ni kwamba ili Bunge liweze kumlipia Lissu matibabu yake ni lazima taasisi hiyo iwe imepata barua hizo tatu za vibali! Hili ndilo shimo ambalo Spika Ndugai alishajichimbia kwenye mjadala wa Bunge kuwajibika kumtibu Lissu!
Ndiyo maana wengine tulipoona nukuu za awali leo (kabla ya masahihisho) kuwa Spika Ndugai amezungumzia kuhusu malipo ya matibabu ya Lissu na kwamba Bunge limetoa fedha kulipia, tulijuliza kuna muujiza mwingine umetokea katika 'uhai' wa Lissu baada ya ule muujiza wa kuokoka kwenye shambulio la kikatili?
Iwapo Spika ataweza kujitoa yeye na mhimili huo katika 'shimo' la vibali na barua tatu, utakuwa ni mojawapo ya muujiza mwingine katika matibabu na uponaji wa Lissu!
Hivyo basi tumuachie muda Spika Ndugai aandae mkeka wake vyema, akitambua kuwa jambo ambalo Lissu amekuwa akilirudia kulisema tena na tena na tena, kila mahali ni kwamba Bunge halijawahi kumlipa hata senti moja ya gharama za matibabu yangu.
Mkeka wa Spika Ndugai unapaswa kujielekeza kwenye madai hayo ya 'hata senti moja'! Vinginevyo aitoe kwanza taasisi hiyo kwenye shimo la barua tatu za vibali, kisha atakuwa huru kuzungumzia matibabu ya Lissu na mkeka wake utakuwa na maana!
*Tumaini Makene*
*Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano*
*CHADEMA*
Hivyo makala CHADEMA WAMJIBU SPIKA NDUGAI MALIPO MATIBABU YA LISU.
yaani makala yote CHADEMA WAMJIBU SPIKA NDUGAI MALIPO MATIBABU YA LISU. Wakati huu, pengine unaweza kutoa faida na wewe wote. Sawa, kuona katika post nyingine makala.
Wewe ni sasa kusoma makala CHADEMA WAMJIBU SPIKA NDUGAI MALIPO MATIBABU YA LISU. mahali kiungo https://wordmaelezo.blogspot.com/2019/01/chadema-wamjibu-spika-ndugai-malipo.html
0 Response to "CHADEMA WAMJIBU SPIKA NDUGAI MALIPO MATIBABU YA LISU."
Post a Comment