title : PAUL KIMITI: BW. KILIMO, MWANAMUZIKI, DJ, MTANGAZAJI, MKUFUNZI NA MZALENDO ALIYEWAHI KUWA WAZIRI NA RC KWA WAKATI MMOJA!!!
kiungo : PAUL KIMITI: BW. KILIMO, MWANAMUZIKI, DJ, MTANGAZAJI, MKUFUNZI NA MZALENDO ALIYEWAHI KUWA WAZIRI NA RC KWA WAKATI MMOJA!!!
PAUL KIMITI: BW. KILIMO, MWANAMUZIKI, DJ, MTANGAZAJI, MKUFUNZI NA MZALENDO ALIYEWAHI KUWA WAZIRI NA RC KWA WAKATI MMOJA!!!
1. Usuli:
Mh. PAUL PETER KIMITI alizaliwa tarehe 15.1.1940 mkoani Rukwa.
2. Elimu:
Mh. KIMITI alipata elimu ya msingi mkoani Rukwa kabla ya kujiunga na shule ya sekondari ya Mzumbe kwa masomo ya sekondari mwaka 1954.
3. Kuanza Kazi akiwa "Teenager":
Mh. KIMITI, mara tu baada ya kumaliza elimu ya sekondari, akiwa kijana mdogo wa miaka 19 tu, aliajiriwa Wizara ya Kilimo kama "Extension Officer" mwaka 1959. Licha ya umri wake mdogo, Mh. KIMITI aliheshimika kutokana na siku zote kufanya kazi kwa bidii.
4. Kujiunga na TENGERU Agricultural College"
Mh. KIMITI alijiunga na chuo hiki kilichopo "A-Town" mwaka 1961 kwa minajiri ya kuongeza "madini" kichwani Mh. KIMITI akawa pia Mwenyekiti wa chama cha wanafunzi chuoni hapo kutokana na karama yake kubwa ya uongozi aliyojaaliwa na Mola wake.
5. Kupata "Zali" la kwenda "Mamtoni"
Mh. KIMITI alikuwa mmoja wa Watanganyika wa mwanzo kupata "Scholarship" kwenda kusoma n'gambo pale alipokwenda chuo cha Deventer, Uholanzi mwaka 1962 kusomea Kilimo.
6. Kuanzisha Bendi ya Muziki Uholanzi:
Mh. KIMITI, akiwa nchini humo, alibahatika kukutana na Mbongo toka Mkoani Kilimanjaro akiitwa ALPHONCE LYIMO. Wabongo hao wakawa marafiki walioshibana huku wakiwa ni wapenzi wakubwa wa muziki hivyo wakaanzisha bendi yao waliyoiita "Safari Brothers". Mh. KIMITI alikuwa mwimbaji huku pia akivurumisha gitaa kwa ustadi wa hali ya juu na kukonga nyoyo za watu wengi. Bendi hiyo ikatokea kuwa maarufu sana na ilikuwa na nyimbo nyingi zilizopendwa na watu wa mataifa mbalimbali.
7. Kukutana na Rais NYERERE:
Mh. KIMITI alikutana na Mwalimu NYERERE kwa mara ya kwanza mwaka 1965 huko Uholanzi. Mwalimu alikuwa katika harakati zake za kuzungukia mataifa mbalimbali ili kuliletea maendeleo taifa lake changa. Mh. KIMITI na Bw. LYIMO walimkabidhi Mwalimu £ 20,000 kupitia "Tanganyika Development Fund" kama mchango wao kwa taifa lao jipya. "mbumba" hizi, ambazo zilikuwa ni nyingi mno wakati huo, zilitokana na mauzo ya rekodi zao za muziki.
8. Kurejea Bongo:
Mh. KIMITI, tofauti na wabongo wengi enzi hizo waliokuwa na kasumba ya "kuzamia" na "kulowea" "majuu", baada ya kuhitimu mafunzo yake, alirejea nchini mwaka 1965.
9. MKUFUNZI Ukiriguru Agricultural Institute:
Mh. KIMITI akaanza kuhudumu chuo hiki kilichopo Mwanza akiwa Mkufunzi. Kwavile "Jasili haachi asili", Mh. KIMITI, akiwa chuoni hapo, akaanzisha bendi aliyoiita "Crooning Stars" na baadaye aliibadili na kuiita "Luna Fiesta" kutokana na kwamba wakati huo wanaanga wa US walikuwa wamekwenda mwezini mwezi Julai, 1969 ambayo ndio ilikuwa "habari ya mujini" wakati huo.
10. Kuhamishiwa Makao Makuu ya TANU:
Mh. KIMITI alihamishiwa Makao Makuu ya TANU kama Katibu Msaidizi baada ya Mwalimu NYERERE kugundua talanta yake kubwa kwenye tasnia hiyo.
11. Kuwa DJ na Mtangazaji:
Moja ya majukumu yake makubwa akiwa Makao Makuu ya TANU ilikuwa kuandaa program za mafunzo ya siasa kwa wana-TANU. Mh. KIMITI akawa akifundisha makuruta kambi za JKT, wanafunzi mashuleni na vyuo mbalimbali ikiwemo Udsm. Aidha, alikuwa DJ na Mtangazaji aliyeandaa na kutangaza vipindi vya siasa mf "The Rise of TANU", "TANU katika Historia" nk na kupiga nyimbo za kizalendo za kuwalaani mabeberu huku "akifagilia" siasa ya ujamaa na kujitegemea.
12. Cheti cha "Labour Movement"
Mh. KIMITI, kati ya mwaka 1969 na 1970, alikwenda Ujerumani kwenye kozi na kutunukiwa cheti "Certificate in Labour Movement".
13. Kusomea Shahada ya Uzamili US:
Mwaka 1973, Mh. KIMITI, ambaye daima huamili elimu ndio mkombozi wa mwanadamu, alikwenda chuo cha Calpoly, California, US kwaajili ya kozi ya "Masters" ya "Agricultural Science".
14. MKUU wa Uyole Agricultural Institute:
Mh. KIMITI aliporejea Bongoland toka Marekani akawa Mkuu wa chuo hiki kilichopo mkoani Mbeya toka 1975 hadi 1979.
15. MKUU wa Nyegezi Agricultural Institute:
Mh. KIMITI alihamishiwa chuo hiki na kuhudumu toka 1979 hadi 1982.
16. Mh. KIMITI kuwa "Nominated MP":
Mh. KIMITI alienda jimboni Sumbawanga mjini kwaajili ya kinyanganyiro cha ubunge wa taifa na jina lake likawa moja ya majina matatu yaliyofikishwa kwenye vikao vikuu vya CCM Idodomia kupigiwa kura na hatimaye yeye akaibuka mshindi.
17. Rais NYERERE amteua kuwa WAZIRI:
Mwalimu NYERERE alimteua Mh. KIMITI kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu mwaka 1982. Hii ilikuwa ni heshma kubwa kwake.
Mh. KIMITI akaanza kufanya kazi chini ya Waziri Mkuu wa wakati huo, Mh. CLEOPA DAVID MSUYA na baadaye chini ya "mwanamume wa shoka" marehemu EDWARD MORINGE SOKOINE, ambaye ukimuondoa Mwalimu NYERERE, ndiye aliyekuwa kipenzi cha watanzania kutokana na utendaji kazi wake mujarab na uadilifu usio na mfanowe.
18. SOKOINE amwambia KIMITI asome somo Kanisani:
Kwenye mkesha wa mwaka mpya 1984, Waziri Mkuu SOKOINE alimwambia Mh. KIMITI pamoja na mawaziri wengine wawili Bi. ANNE MAKINDA na Bi. ANNA ABDALLAH, waliokuwa chini yake, kwenda kanisa la Mtakatifu Joseph kwaajili ya kusoma masomo kanisani hapo ili kuonesha kwamba mawaziri nao hushiriki kikamilifu mambo ya kiimani. Katika usiku huo wa kihistoria, mawaziri hao 3 walikonga nyoyo za mapadri na waumini kwa jinsi walivyokuwa wakitiririka neno la Mungu kwani walizoeleka kuonekana kwenye viunga vya siasa tu.
19. "Mtiti" na Rais NYERERE:
Mwalimu NYERERE hakuwa na msalie mtume na mtu yeyote kwenye masuala ya uadilifu hata awe ni rafiki yake kiasi gani.
Siku moja, Mwalimu alipata habari kwamba Mh. KIMITI anajenga nyumba kubwa hapo Idodomia. Mara moja, Mwalimu akamwita Mh. KIMITI na kumuweka "kitimoto".
Mwalimu, huku akiwa ameghadhabika lakini akiwa makini sana, akamuuliza Mh. KIMITI:
"Paul, wewe ni Waziri wangu. Najua mshahara wako ni TZS 5,000/= tu, unajenga nyumba hiyo umepata wapi hela wewe?".
Mh. KIMITI, akamweleza Mwalimu kinaganaga na kwa ufasaha mkubwa, huku akichambua nyaraka lukuki, kwamba hiyo ni nyumba anayoijenga kwa mkopo wa THB.
Mwalimu aliridhika kabisa na majibu hayo kuntu ya Mh. KIMITI na kuanza kutoa vichekesho vyake, kama kawaida yake, huku akicheka na kisha akamruhusu Mh. KIMITI akaendelee kuchapa kazi.
20. Mwalimu NYERERE amteua kuwa RC Kilimanjaro:
Mwaka 1984, Mwalimu alimteua Mh. KIMITI kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ambapo wakiwa Ikulu, Mwalimu alimwambia:
"Paul, nimekuteua kuwa RC Kilimanjaro na wajibu wako mkubwa kule nataka ukaanzishe kilimo cha kisasa".
Mh. KIMITI alitekeleza maagizo hayo kwa ufanisi mkubwa ambapo alileta mabadiliko makubwa ya kilimo. Aidha, alisimamia "Lower Moshi Irrigation Project" na kuagiza matreka "Kubota" 200 toka Japan yaliyosaidia sana maendeleo ya kilimo mkoani humo. Mh. KIMITI alihudumu mkoani humo hadi 1989.
21. Rais MWINYI amteua RC Kagera:
Mwaka 1989, Rais wa awamu ya 2 Alhaj ALI HASSAN MWINYI "Mzee Rukhsa" alimteua Mh. KIMITI kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera ambako alihudumu hadi mwaka 1991.
22. Rais MWINYI amteua kuwa RC Mbeya:
Mwaka 1991, Rais MWINYI alimteua Mh. KIMITI kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambako aliacha "legacy" kutokana na barabara nyingi za lami zilizojengwa vitongoji mbalimbali vya jiji hilo katika kipindi cha uongozi wake.
Miradi mingi aliyoibuni na kuisimamia akihudumu kama Mkuu wa Mkoa katika mikoa yote aliyopitia ilitokana na kuhamasisha wananchi kujitolea kwa michango ingawa miradi mingine ilitekelezwa na serikali.
23. Kugombea Ubunge Simbawanga Mjini:
Kwa miaka yote toka 1980, Mh. KIMITI alikuwa ni "Nominated MP". Mwaka 1995 akaamua kwenda kugombea jimboni na kutokana na kupendwa na wananchi, akaibuka kidedea.
24. Mwalimu NYERERE amuuliza Mh. KIMITI kama anagombea Urais 1995!
Tarehe 30.4.1995, Mwalimu NYERERE 'alitia timu" jijini Mbeya kwaajiri ya sherehe za Mei Mosi zilizokuwazimepangwa kufanyika mkoani humo kitaifa.
Mwalimu alikuwa na maongezi na Mh. KIMITI siku hiyo ambapo alimuuliza kama alikuwa ana mpango wa "kutia nia" kugombea Urais kwani uongozi wa Rais MWINYI ulikuwa unagota mwishoni mwa 1995 kwa mujibu wa Katiba ya nchi.
Mh. KIMITI, kwa heshma na unyenyekevu wa hali ya juu, alimjibu Mwalimu:
"Hapana, Mwalimu. Mimi najiona sistahili kugombea nafasi hiyo kwani Urais ni kazi ngumu sana".
Mwalimu alivutiwa na majibu ya Mh. KIMITI hivyo wakaendelea na mazungumzo mengine kuhusu maendeleo na changamoto za jiji la Mbeya na nchi kwa ujumla.
Kesho yake, tarehe 1.5.1995, Mwalimu alikuwa mgeni wa heshma kwenye sherehe za Mei Mosi kitaifa, uwanja wa Sokoine, ambapo alitoa hotuba ya kihistoria kuhusu kukimbilia Ikulu. Mwalimu alisema: "Ikulu ni mahali patakatifu. Ikulu si mahali pa kukimbilia hata kidogo na watu makini hawapakimbilii".
25. Kuwa WAZIRI na RC Kwa Wakati Mmoja!
Rais wa awamu ya 3, Mh. BENJAMIN WILLIAM MKAPA alimteua Mh. KIMITI kuwa Waziri wa Kilimo mwaka 1995 hadi 1998 alipomteua kuwa Waziri wa Kazi na Vijana.
Mwezi Octoba, 1997 taifa lilipopata msiba mkubwa Mwalimu NYERERE alipofariki, Mh. KIMITI alipewa heshma kubwa ya kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi ya Baba wa Taifa. Kwa hakika, lilikuwa ni jukumu kubwa sana ambalo Mh. KIMITI alilitekeleza kwa weledi wa hali ya juu na kupelekea Baba wa Taifa kupata mazishi yaliyomstahili. Kwakuwa RC NIMROD LUGOE alikuwa mgonjwa, Rais MKAPA alimteua Mh. KIMITI kukaimu nafasi ya Ukuu wa Mkoa ili awezekufanya kazi kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mkoa wa Mara.
Mh. KIMITI akakonga nyoyo za waombolezaji toka mataifa mbalimbali pale alipouvua u-Waziri na u-RC na kuingia "fronti" kanisani na kaburini kwa kuwa MC ambapo aliendesha shughuli hiyo kwa umahiri wa hali ya juu na kuwafurahisha vilivyo waombolezaji akiwemo Rais MKAPA!.
Mwezi desemba 1999, Rais MKAPA alimteua Mh. KIMITI kumpokea jijini Mwanza na kisha kuongozana hadi kaburini Butiama, Rais NELSON MADIBA MANDELA, Kiongozi Bora kabisa Duniani kwa Karne ya 20 ambaye hata Umoja wa Mataifa umeitenga siku maalum kwaajili yake "Nelson Mandela International Day"(Tarehe 18 Julai ya kila mwaka ambayo pia ni Birthdate yake). Mh. KIMITI alimsindikiza Mzee MANDELA kaburini na kwake Mh. KIMITI hii ilikuwa ni heshma kubwa sana.
26. Kushinda kwa Kishindo Ubunge 2005:
Mh. KIMITI aligombea tena ubunge wa jimbo la Sumbawanga mjini mwaka 2005.
Mh. KIMITI alipata kura 37,019(88%) huku akiwatimulia vumbi mgombea wa CHADEMA; Bi. HONORATA aliyeambulia kura 3,901(9%) na wa CUF aliyeambulia 2.7%, ikionesha wazi vyama vya upinzani vilikuwa "vinapumulia mashine" jimboni humo!.
27. Kung'atuka Ubunge 2010:
Mh. KIMITI ni mmoja wa viongozi wachache sana "wanaomuishi" kivitendo Baba wa Taifa tofauti na viongozi wengi "wanaomuishi" Mwalimu "kimagumashi" kimaneno. Mh. KIMITI alidhihirisha hilo alipoamua, kama alivyofanya Mwalimu NYERERE mwaka 1985, kung'atuka ambapo tarehe 8.1.2010 alisema:
"Ni vizuri ukaondoka madarakani ukiwa na nguvu huku bado ukipendwa. Kamwe usisubiri watu wakuchoke".
Tarehe 13.7.2010, Mh. KIMITI na mbunge mwenzake wa Sumbawanga, Mh. CHRISSANT MAJIYATANGA MZINDAKAYA waling'atuka rasmi na waliaga bungeni na kushangiliwa mno.
Katika uchaguzi uliofanyika tarehe 25.1.2010, baada ya Mh. KIMITI kung'atuka, CCM "ilitokea dirishani" jimboni Sumbawanga mjini baada ya mgombea wake Mh. AIESH HILARY kuchomokea kupitia tundu la sindano kwa kupata kura 17,328 (48.99%) na kumshinda mgombea wa CHADEMA Bw. YAMSEBO JOSEPH aliyepata kura 17,132 (48.44%)!!!.
28. Kujiuzulu Bodi ya ATCL kutokana na "Mafindofindo"
Katika muendelezo wake wa uzalendo na uadilifu, mwaka 2009, Mh. KIMITI aliamua ghafla kujiuzulu ujumbe wa Bodi ya ATCL baada ya kuhudumu toka 2007. Hii ilikuwa ni baada ya kutokubaliana na uamuzi wa Menejinenti ya ATCL kuamua kukodi ndege ya Airbus 320-214 kutoka kampuni ya Wallis Trading kinyume cha sheria bila kuihusisha Bodi huku Waziri mhusika akionekana kulifumbia macho suala hilo.
29. Mh. KIMITI na Maombi ya Dr. KULOLA
Mh. KIMITI alikuwa na ukaribu na marehemu Askofu Mkuu EAGT, Dr. MOSES KULOLA. Hili lilibainika wakati wa kuaga mwili wa askofu huyo jijini Dsm tarehe 31.8.2013 ambapo Mh. KIMITI alitiririka: "Marehemu baba Askofu KULOLA aliniombea ofisini kwangu wakati huo nikiwa RC Kilimanjaro. Mbele ya bendera ya Taifa nilipiga magoti na mtumishi huyu aliyekuwa akitembea na Yesu akaniombea sana. Kwa maombi yake nilifanikiwa kuwa Waziri kwa vipindi viwili na almanusra niupate UWAZIRI MKUU".
30. Kuwa Mbunge Bunge la Katiba
Mh. KIMITI alishiriki na kutoa mchango mkubwa wakati wa mchakato wa kuundwa kwa Katiba mpya bungeni ambapo alikuwa Mwenyekiti wa Kamati na. 12.
31. Rais JPM amteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi:
Tarehe 16.10.2018, Rais wa awamu ya 5, Mh. Dr. JOHN JOSEPH POMBE MAGUFULI alimteua Mh. KIMITI kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ranchi za Taifa NARCO baada ya kuona Taifa bado linahitaji huduma za mgongwe huyu nguli.
Huyu ndiye PAUL PETER KIMITI, Mzalendo mwadilifu, mwenye familia yenye watoto 4 ambapo 3 ni wavulana na 1 msichana, aliyeteuliwa na Rais NYERERE kuwa Waziri na RC, Rais MWINYI kuwa RC, Rais MKAPA kuwa Waziri na RC na Rais MAGUFULI kuwa Mwenyekiti wa Bodi.
Hivyo makala PAUL KIMITI: BW. KILIMO, MWANAMUZIKI, DJ, MTANGAZAJI, MKUFUNZI NA MZALENDO ALIYEWAHI KUWA WAZIRI NA RC KWA WAKATI MMOJA!!!
yaani makala yote PAUL KIMITI: BW. KILIMO, MWANAMUZIKI, DJ, MTANGAZAJI, MKUFUNZI NA MZALENDO ALIYEWAHI KUWA WAZIRI NA RC KWA WAKATI MMOJA!!! Wakati huu, pengine unaweza kutoa faida na wewe wote. Sawa, kuona katika post nyingine makala.
Wewe ni sasa kusoma makala PAUL KIMITI: BW. KILIMO, MWANAMUZIKI, DJ, MTANGAZAJI, MKUFUNZI NA MZALENDO ALIYEWAHI KUWA WAZIRI NA RC KWA WAKATI MMOJA!!! mahali kiungo https://wordmaelezo.blogspot.com/2019/01/paul-kimiti-bw-kilimo-mwanamuziki-dj.html
0 Response to "PAUL KIMITI: BW. KILIMO, MWANAMUZIKI, DJ, MTANGAZAJI, MKUFUNZI NA MZALENDO ALIYEWAHI KUWA WAZIRI NA RC KWA WAKATI MMOJA!!!"
Post a Comment